SIMULIZI YA NAKUMBUKA TU NA AWADH PALANGU

          
SIMULIZI- NAKUMBUKA TU

MTUNZI- AWADH PALANGU
SIMU: 0713 899 084, 0785 056 575

INSTAGRAM/FB AWADH PALANGU

SHUKURANI
Kwanza ninapenda kumshukuru Allah mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniajalia siha njema na uwezo wa kuandika kitabu hiki. Nawashukuru  walimu wangu wa sarufi na fasihi kwa kunijengea msingi na kunipa maarifa yaliyoniwezesha kuandika kitabu hiki, namshukuru Mwalimu Muhango wa chuo kikuu mkwawa, Mwalimu Tito mgani mwalimu  wa kiswahili shule ya sekondari mwakavuta, wafanyakazi wa makumbusho ya Mkwawa-kalenga pia namshukuru Muslim Kalilo kwa kubuni na kuchora kifuniko cha kitabu hiki kwa usanifu. Shukurani za pekee kwa wazazi wangu na familia yangu kwa ujumla kwa mchango wao wa hali na Mali. Shukurani zangu pia nazitoa kwa wale wote waliosaidia kitabu hiki kikamilike. Allah awafanyie wepesi katika kila jambo la kheri.

UTANGULIZI
Riwaya ya nakumbuka tu ni riwaya inayoelezea mikasa na visa mbalimbali vya mapenzi amabvyo vilivyomkumba Samir. Samir ni kujana aliyepitia changamoto kadha wa kadha katika suala zima la mahusiano na mpenzi wake Nancy na hatimaye kupelekea kuvunjika kwa mahusiano hayo ingawa mahusiano hayo yaliharibika lakini Samir bado alikuwa anampenda sana Nancy, alitumia muda wake mwingi sana kukumbuka maisha ya mahusiano yao yalivyokuwa. Je unajua ni vitu gani Samir alivyokuwa anavikumbuka.?, Jibu la swali hii linapatikana katika riwaya hii ya NAKUMBUKA TU, karibu uisome.
Nakumbuka miaka kadhaa iliyopita wakati nilipokuwa nasoma shule ya msingi Windini iliyopo mjini Ifakara. Nilifurahia sana maisha ya shule kwani yalikuwa ni yenye kuvutia mno hususani nikikumbuka michezo mbali mbali tuliyokuwa tunachecheza kama vile mpira wa miguu, netball pamoja na michezo mingine mingi.
Nakumbuka pia jinsi mwalimu Kabata alivyokuwa anatufundisha nyimbo mbali mbali ambazo tulizokuwa tunaimba, mfano tuliimba wimbo wa shule pamoja na nyimbo za uzalendo kama vile Tazama ramani,Tanzania nakupenda kwa moyo wote na wimbo wa Taifa wa nchi yetu, ama kwa hakika nimeyakumbuka sana maisha ya shule. Nilikuwa nafurahishwa sana pale tulipokuwa tunakaa mstalini halafu baadhi ya wanafunzi walikuwa wanapiga ngoma (bendi) huku wengine tukiimba. Siku ya Juma tatu na alhamisi nakumbuka ilikuwa ni siku ya usafi ambapo katika siku hiyo walimu walikuwa wakiwatoa mbele wanafunzi wote wachafu, hapo bendi ilipigwa kwa kuzingatia wimbo wa kama mchafu toka mbele.
Nancy ni msichana aliyekuwa anasoma na mimi darasa moja. Siku zote walimu walimsifia sana kwa usafi hakika alikuwa anang'aa kwa usafi wake. Alikuwa haji shule bila kunyosha sare zake za shule, shati lake jeupe lilikuwa linampendeza sana. Ukweli ni kwamba nilivutiwa sana na usafi wa msichana huyo.
Nancy hakuwa tu mwanafunzi mwenzangu bali pia alikuwa jirani yangu kwa maana ya kwamba tulikuwa tunakaa Mtaa mmoja.  Rangi yake nyeusi iliwavutia sana watu, wengi walimuita black beauty, japokuwa alikuwa hafugi nywele Lakini pamoja na kuwa alikuwa ananyoa Mara kwa Mara bado alionekana kuwa ana nywele nzuri nyeusi asilia. Sitaki kuzungumzia sana muoneko wake na uzuri wa Nancy lakini itoshe kusema tu alikuwa mzuri mithili ya malaika. Upande wa taaluma pia hakuwa nyuma, alikuwa anafanya vizuri darasani hususani katika somo la hisabati.
Nancy alikuwa ananionea huruma sana pale nilipokuwa napewa adhabu na mwalimu hususani adhabu ya viboko. Mara nyingine alikuwa anatoa hata machozi pale aliponiona nalalamika kuumia nikiwa naadhibiwa. Sijui ni kwasababu tulikuwa tunakaa Mtaa mmoja au sijui kwasababu alikuwa rafiki yake na Dada yangu (mtoto wa shangazi) aliyefahamika kwa jina la  Tedy ambaye pia tulikuwa tunasoma naye darasa moja, sijui ni kwasababu tu ya upendo wake kwangu ambao ndio uliomfanya awe hivyo. Nilijiuliza sana lakini sikuweza kufahamu
Nakumbuka tulipoingia darasa la sita, rafiki yangu Bryan aliniambia kwamba.
"Samir huyu manzi atakuwa anakupenda, si bure! Wewe unatakiwa uelewe kwa vitendo tu, mwanamke huwa mgumu sana kueleza hisia zake kwa maneno lakini utamgundua kupitia vitendo vyake, amka Samir chukua mzigo huo"
Maneno hayo ya rafiki yangu Bryan kwakweli yaliamsha hisia zangu na kuhisi kweli Nancy atakuwa ananipenda lakini nilikuwa nashindwa jinsi ya kuanza kumuelezea hisia zangu, yaani kumtongoza, ila kabla hata ya Mimi kumtongoza Nancy watu walishaanza kuhisi kuwa sisi ni wachumba kufuatia matendo yetu kama vile kuangaliana mara kwa mara pamoja na matendo mengine.
Kimsingi nilikuwa napata mtihani kumueleza Nancy hisia zangu. Baada ya kutoka shule basi Mara kwa Mara nilikuwa napita nyumbani kwa Nancy ili hata nimuone tu. Niliridhika pia kuona hata sare zake za shule alizokuwa anazifua na kuzianika. Hata nisipomuona yeye ila nilipokuwa nikiziona sare zake tu moyo ulikuwa unafarijika kwa kiasi chake.
Dada yangu (Tedy) ambaye ni Dada binadamu alikuwa akimtania Nancy kwa kumuita Wifi. Hali hii ya mzaha kama huu ilienea na hata wanafunzi wengine walikuwa wakisikia na kujiaminisha kile wanachohisi kuhusu mahusiano ya mimi na Nancy. Siwezi kusahau Mara ya kwanza nilipomtamkia Nancy kuwa ninampenda na kwamba ninamhitaji kwa mapenzi. Lo! Nancy alinikatalia katu!, kitu ambacho sikutaka kuamini kwa wepesi kwakweli. Lakini kukataa kwake kulionekana kutokana na woga kwani wote tulikuwa bado hatujaanza kujihusisha na masuala ya kimapenzi. Hivyo Nancy alinikatalia na kuniambia kwamba yeye bado mdogo na kwamba anaogopa kufanya jambo hilo.
Japo alinikatalia lakini bado jibu lake halikunikatisha tamaa sana nilizidi kumfuatilia Nancy mpaka tulipoingia darasa la saba.
"Samiri Mimi naogopa kufanya bwana! We subiri nikue kidogo mpaka tufike sekondari."
Hili lilikuwa jibu lingine alilonipa Nancy kwa mara ya pili, basi ilibidi niendelee kuishi kwa matumaini huku nikitamani tumalize haraka shule ya msingi.
Siku hazigandi baada ya miezi mitano tukamaliza shule ya msingi lakini kwa bahati mbaya baada tu ya kumaliza shule ya msingi Nancy alisafiri kuelekea Dar es salaam. Hivyo ikawa changamoto tena kwa Mimi kuweza kukutana naye, lakini kabla hajarudi Kutoka Dar kuja Ifakara, Mama yake pamoja na ndugu zake wengine waliamia kwenye nyumba yao huko Mtaa wa Uhuru ambapo ni mbali kidogo na Mtaa niliokuwa nakaa tena kwa bahati mbaya mimi sikufahamu kama mama yake ameamia mtaa gani.
Nancy alikaa huko mpaka majibu yalipotoka, alifauru kwenda shule ya sekondari Kiyovile na hapo ndipo aliporudi moja kwa moja na kufikia kwa mama yake. Wakati huo mimi nilikuwa sifahamu kama yeye amerudi, mimi pia niliendelea na shule kwa ngazi ya sekondari ambapo hapa sasa tulikuwa tunasoma shule tofauti.
Kulingana na hali hiyo ilipelekea mimi kuanzisha mahusiano na binti mmoja hapo mtaani kwetu. Kimsingi sikumpenda msichana huyo lakini kwasababu tu ya kukidhi haja ya mihemko nilijikuta nimeingia kwenye couple isiyokuwa sahihi. Akili yangu na mawazo yangu yote yalikuwa kwa Nancy.
Basi sikubahatika tena kuonana na Nancy mpaka tulipomaliza kidato cha nne. Baada ya kumaliza kidato cha nne Nancy alisafiri kwenda tena Dar es salaam. Mimi pia nilisafiri kuelekea Dar es salaam lakini muda wote huo nilikuwa bado sifahamu kwamba Nancy yupo wapi?. Nilikaa Dar es salaam mpaka majibu ya form four yalipotangazwa kwa bahati nzuri nilifaulu na kwamba nilitakiwa niendelee na shule kwa ngazi ya kidato cha tano na sita yaani advance level.
Nancy aliendelea kubaki Dar es salaam hata baada ya majibu kutangazwa. Yeye hakupenda kuendelea na kidato cha tano japo ufauru wake ulimruhusu, lakini kutokana na ushauri aliopewa na Dada yake na yeye pia aliuafiki.
"Nancy Mdogo wangu! Kutokana na hali halisi ya maisha hapa nyumbani binafsi nakushauri usiende form five ila nenda college moja kwa moja ukasomee taaluma yoyote na hapa napendekeza hotel management au teaching(ualimu). Elimu haina mwisho kama utataka kujiendeleza basi utafanya hivyo wakati upo kwenye ajira yako tayari. Nancy unaona maisha halisi hapa nyumbani baba yetu ndio hivyo ametutoka tangu wewe ulipomaliza darasa la saba. Hivyo mama hapa ndiye pekee aliyebaki kama mtetezi wa maisha yetu, tambua mama hana kazi Nancy anajitahidi kujishughulisha na kilimo ili tu sisi tupate kula pamoja na mambo mengine, halafu mbaya zaidi upande wa baba karibu ndugu zetu wote wametutenga! Hawakumbuki kabisa kama ndugu yao aliacha watoto. Haya maisha inabidi tuwe makini Mdogo wangu, tambua hatuna msaada sehemu yoyote hapa tulipo kuna baadhi ya ndugu upande wa baba wanapenda kutusaidia lakini wanaogopa kutengwa na ndugu zao.(anaendelea kuongea huku akilia) Nancy Mdogo wangu okoa jahazi hili. Mimi nimejishikisha tu na kazi hii ya ufundi kushona lakini changamoto zake ni nyingi kwani hata cherehani yenyewe siyo yangu. Naomba niishie hapo Mdogo wangu".

Mara baada ya kuongea maneno hayo Nancy pia aliangua kilio kisha akamjibu Dada yake (Monarisa) kuwa "Nimekuelewa Dada, umenieleza maneno yaliyogusa hisia zangu, hakika nimekuelewa Dada. Mimi ningependa kusomea Hotel management".
Baada ya hapo ni kweli Nancy alisomea hotel management. Alipomaliza chuo hakubahatika kupata ajira alikaa nyumbani karibu mwaka mzima hivyo akaamua kujiunga na dada yake kujifunza ufundi wa kushona nguo. Alipata umaurufu sana kupitia kazi hiyo pia alipatia sana kushona nguo za kike.
Lakini baada miezi mitatu hivi Nancy aliingia katika mahusiano na jamaa Fulani aliyejulikana kwa jina la Mubaraka.
Mubaraka ni kijana anayetokea kwenye familia iliyokuwa na imani thabiti ya dini ya kiislamu. Wakati huo wote mimi nilikuwa nipo chuo kikuu cha Dar es salaam nikisomea shahada ya Sheria. Nilipomaliza chuo nilirudi nyumbani lakini bado mawazo yangu hayakuweza kuhama kwa msichana aliyetawala hisia zangu. Nilimtafuta kwenye mitandao yote ya kijamii niliyojiunga kama vile Facebook, Instagram na Twitter sikuweza kumpata kwani alitumia jina tofauti kabisa.

Siku moja kama bahati tu naingia Facebook nakuta friend request ya Nancy lakini alitumia jina tofauti niliweza kumgundua kwasababu ya Picha yake aliyoiweka profile.
Nilifurahi sana kwani nilihisi sasa muda wa kuwasiliana tena na Nancy umefika baada ya kupotezana kwa muda mrefu.
Nilipokubali tu ombi lake la urafiki sikusita kumtumia meseji inbox. Hata yeye pia alionekana kuwa na furaha sana, hatukuchati sana kupitia Facebook akaniomba namba za simu nami nikampatia, akanambia badae atanitafuta, basi tukaagana kwa muda ule.
Baada ya kama saa mbili hivi nikaona meseji ya WhatsApp kwenye simu yangu, nilipoangalia namba haikuwa kwenye kitabu cha namba cha simu yangu yaani namba ngeni. Lakini sikufikiria kama angekuwa Nancy kwani kodi namba za namba zile zilikuwa si za Tanzania.
Alianza kwa kunisalimu "mambo!"
Nikamjibu “Poa akatuma tena meseji nyingine "mbona kimya sana?"
Nikamjibu samahani sijajua nachati na nani?
"Mimi ni mpenzi wako unipandae yaani mkeo mtarajiwa"
"Mmh! Embu acha utani bana wewe nani taja jina lako"
"Aaah! Kumbe tupo wengi eeehh Samir!, leo kukubadilishia namba tu unajifanya hunijui"
"Sasa sikia Mimi sitaki usumbufu kama hutaki kujitambulisha basi usinitumie meseji siwezi kuchati na mtu nisiyemfahamu".
Baada ya kumtumia meseji hii, Nancy akaona bora ajitambulishe.
" Mimi Nancy Egino"
"Oooh! Samahani sana Nancy! Nilikuwa sijakufahamu kabisa yaani nisamehe bure mwenzako".
"Sawa,wala usijali Samir lakini unaonekana kuwa ni mtu makini sana".
"Kwanini Nancy?"
"Kukutania kidogo tu ulitaka uache kuchati na wanaume wengi hawapo hivi, una msimamo sana....good"
"Kawaida Nancy unajua mimi huwa sipendi usumbufu".
Basi tuliendelea kuchati hapo huku kila mmoja akionekana kuwa na hamu ya kumuona mwenzake. Niliomba anitumie Picha zake ili nione muonekano wake kwa muda huo. Ama kwa hakika Nancy alizidi kuwa mzuri zaidi, yaani nilizidi kuchachawa na kupagawa baada ya kuziona picha zake, sikusita kumsifia kuwa amezidi kuwa mzuri. Nancy pia aliomba nimtumie picha zangu nami nilifanya vivo hivyo. Yeye pia alinisifia kuwa nimenenepa na kwamba nimekuwa mzuri pia.
Baada ya kuchati sana Nancy aliniambia anataka anipigie kutumia mtandao wa IMO. Ni kweli alinipigia story zilizidi kupamba moto huku tukikumbushana maisha ya shule na baadhi ya matukio ya kusisimua yaliyowahi kutokea tukiwa shuleni, hakika wote tulionekana kuwa na furaha kubwa sana isiyo kifani. Lakini wakati huo wote kumbuka sauti ya Nancy haikuwa ya kawaida yaani alikuwa akizungumza kwa kutoa sauti fulani nzuri na ya chini kama vile mtu na mpenzi wake wakiwa kitandani na kupiga stori. Kimsingi sikuweza kuvumilia kwakweli kwani aliamsha sana hisia zangu na kujikuta nikiwa katika mhemko mkubwa. Zakari yangu ilikuwa imeshakasirika kufuatia hali hiyo.
Sikusita kumwambia kuwa "una sauti nzuri wewe mtoto yaani mpaka inanipa raha kuisikia zaidi nisikiapo muziki".
Nancy alicheka kidogo kisha akanijibu "kawaida jamani Samir mbona hata wewe una sauti tamu sana inayochoma mpaka kwenye moyo wangu. Nimefurahi sana leo kusikia sauti yako".
Sikujua kama ni kweli alikuwa akimaanisha au la lakini niseme tu nami nilifurahi kusikia ananiambia hivyo. Basi tuliendelea kupiga stori. Kumbuka ilikuwa ni usiku muda wa saa tatu hivi tulianza kuzungumza.
Wakati tunaendelea kuzungumza Nancy aliniuliza
"Nikuulize kitu Samir?"
"Ndiyo niulize tu Nancy
" Lakini Naomba usiniongopee tafadhari niambie tu ukweli"
"Sawa Nancy usijali"
"Samiri una mpenzi?"
"Ndiyo Nancy"
Baada ya kumjibu hivyo nilisikia akisema "Mungu wangu!" Kisha akaendelea kuniuliza
"Naomba niambie ukweli mpenzi wako wa kwanza anaitwa nani? Na umeishi na wasichana wangapi mpaka sasa pia wanaishi wapi hao wasichana na majina yao ningependa niyajue kama hautajali Samir".
Sikutamani kumuongopea kabisa nilikuwa mkweli na muwazi nilimjibu maswali yake yote. Baada ya kumuelezea historia hiyo Mimi pia nilitamani kujua kutoka kwake lakini nilikuwa naogopa kujua historia yake ya mahusiano kwani nilihisi ingeniumiza sana. Binafsi sikutamani kabisa Nancy abikiriwe na mtu mwingine wala aingiliwe na mwanaume yoyote hivyo sikutamani kusikia historia yake ya mahusiano maana ingeniumiza mno. Japo najua ameishi na wanaume wengine lakini sikutaka kujua kiundani.
Nilimwambia tu kwamba mimi natamani kujua historia yako ya mahusiano lakini naogopa kuumizwa na historia hiyo kwani najua itanipa mawazo na maumivu zaidi moyoni. Nancy alinijibu kwamba "wewe niulize tu wala usijali Samir kama utaumia basi nitakufanyia kitu cha kukuondoshea maumivu na mawazo na kukurejesha katika furaha yako".
Basi nikakubaliana naye na akataka kuanza kunisimulia lakini wakati anaanza tu kusimulia simu yangu ilizima, chaji iliisha na siku hiyo walikata umeme hivyo hatukuweza kuwasiliana tena kwa siku hiyo. Asubuhi na mapema baada ya kurudisha umeme nilichajisha simu Kisha nikaingia WhatsApp nikaona ujumbe wake.
"Samiri yaani ndiyo umeamua kukata simu na kuzima kabisa kisa hutaki nikusimulie basi tuachane na hiyo mada tuchat mambo mengine tu".
Nilisikitika sana kuona meseji hiyo. Nilijitahidi kumuelekeza hali ilivyo kwa kumtumia meseji baadae alipoingia online aliona meseji hiyo na kunijibu tu
"Nimekuelewa Samir tutachati vizuri usiku"
Nilitamani jua lielekee magharibi haraka ili basi usiku uingie niweze kuongea na Nancy.
Mara jua likapotea na giza likatanda, ilipotimu saa moja tu mimi nikawasha data nikawa online namsubiria mtoto mzuri Nancy.
Saa moja baadae nikasikia notification ya WhatsApp, nilipoitazama ilikuwa ni meseji ya Nancy.
"Niambie Samir sasa nipo free tunaweza kuchat tu. Nafikiri ni vyema tukazungumza".
Basi alinipigia kupitia IMO tukaanza kubonga. Kabla ya yote nilianza kumuuliza swali la msingi ambalo lilikuwa linanisumbua kichwa nilimuuliza kuwa." Hivi Nancy mbona namba zako za simu siyo za Tanzania? Au haupo Tanzania wewe?"
Nancy alinijibu kuwa "Nipo Tanzania isipokuwa simu hii nilimuagiza mtu ameninunulia nje ya nchi. Sasa imeletwa hapa tayari ilishakuwa na WhatsApp ya mtu aliyekuwa anaitumia kwaiyo hata mimi nilipoweka line yangu WhatsApp namba ikasoma zile zile kwasababu sikubadilisha namba za kutumia akaunti ya WhatsApp na ndiyo maana unaona kodi namba sio za Tanzania".

Baada ya kupata maelezo hayo nilimuelewa vyema, tukaendelea na stori zingine na hapo nilimuuliza lile swali la jana kuhusu historia yake ya mapenzi, kimsingi niliumizwa sana na hadithi hiyo tena zaidi pale aliposema kuwa amezaa ana mtoto mmoja wa kiume...."Dah ilikuwa damu yangu" kimoyo moyo nilijisemea, kisha nilimpa hongera, pia niliumia kwasababu niliona kabisa dalili za kumkosa zinaonekana. Baada ya historia ndefu kumalizika nakumbuka ilikuwa saa saba ya usiku ilibidi nimwambie kuwa nipo hovyo kutokana na historia yake na kwa kuwa yeye aliniahidi kuniweka sawa, basi nikamuachia hiyo kazi ya kunirejesha katika furaha. Unajua alifanya nini? Aisee aliamsha furaha yangu kwa kuniambia.
"I love you Samir, nakupenda siyo masihala bali ninamaanisha uwe mpenzi wangu Samir, amini hivyo ".
Dah! Baada ya kusikia maneno hayo nilihisi kama ninaota maana sikuweza kuamini kwa haraka lakini bado aliendelea kunithibitishia kupitia ulimi wake, basi ilifika pahala nami nikaamini kwamba ni kweli atakuwa anamaanisha. Tukazungumza usiku ule kwa furaha tele mpaka saa tisa ya usiku ndipo tulipoamua sasa tulale tukaaihirisha mazungumzo kwa siku hiyo.

Siku iliyofuata yaani kesho yake asubuhi nilipowasha data nikaingia WhatsApp kwaajili ya kutaka kumsalimia my Darling Nancy lakini nilipoingia nikaiona meseji niliyotumiwa na Nancy " Umeamkaje Samir, baadae nikiwa free kuna kitu nataka nikwambie".
Sikujua ni kitu gani alichotaka kuniambia lakini kwasababu tumeshaingia kwenye makopa basi nikahisi kitakuwa tu kitu kizuri na chenye kupendeza.
Baadae alipopata nafasi, alinitafuta  WhatsApp na kunitumia voice note ambayo ilikuwa na ujumbe ulioumiza moyo wangu.Ujumbe huo ulikuwa hivi "Naomba nisikie kwa makini Samir, Jana nilifanya vile ili tu nikurejeshe katika hali ya kawaida kama ambavyo nilivyokuahidi. Lakini sikumaanisha niliposema kuwa nakupenda kwaiyo mimi naomba uelewe hivyo".
Siwezi kueleza ni namna gani niliumizwa na ujumbe huo lakini itoshe tu kusema kwamba niliumizwa sana, nilifikiri na kuona labda kwakuwa huyu ni mtoto wa kike kwahiyo anatakiwa kubembelezwa na kuelezwa maneno matamu ili basi aweze kunielewa, nikajikaza kiume na kuamua kumueleza kwamba.
"Hapana Nancy usifanye hivyo utakuwa umeniathiri sana tena sana kwani ni bora usingeniambia kuwa unanipenda kuliko hivyo ulivyonifanyia halafu unakuja kunikatalia tena!. Mimi siwezi kukuelewa kabisa yaani Nancy".
Nilipomtumia meseji hiyo Nancy pia alijibu kwa kutoa maelezo ambayo yalizidi kuninyong'onyesha.
"Sikia Samir, Yaani siyo kwamba Mimi nakukatalia tu bali kulingana na hali halisi. Mimi sasa hivi sihitaji kujiingiza kwenye mahusiano nimeona bora nipumzike tu hata hivyo mimi Nina mtoto nimezaa na jamaa fulani, na huyo jamaa wala sijaachana naye isipokuwa tumetengana na imeshindikana kufunga ndoa kwasababu yeye ni muislamu na Mimi ni mkristo kwahiyo kila mtu hakutaka kubadili dini kumfuata mwenzake ili tuweze kufunga ndoa. Lakini kitu kingine mimi sitaki kuingia tu kwenye mahusiano kisha nikaishia njiani napenda tufunge ndoa. Sasa wewe utakubali kufunga ndoa na Mimi wakati nina mtoto halafu pia wewe dini utakubali kubadili ili tufunge ndoa? Maana isiwe nilichokimbia kule nije kukutana nacho kwako.Niambie sasa nikuelewe".
Kimsingi baada ya kunieleza hivyo niliishiwa pozi kwani mimi pia sikuwa tayari kubadili dini. Hivyo nikamjibu tu kama hutaki hata mahusiano ya kawaida tu basi isiwe taabu. Nancy aliniambia kuwa tuendelee tu kuchati kama marafiki tu wa kawaida, ilibidi nikubaliane naye tulikuwa tunachati lakini hatukuwa na stori sana kama zamani. Hivyo hali ile ilimuumiza hata Nancy na kuamua tu tuwe wapenzi na kuhusu suala la dini na mtoto tutalijadili huko baadae.
Nilifurahishwa sana na uamuzi wa Nancy furaha yangu iliyopotea ilirejea tena. Basi tuliendelea na mapenzi yetu huku tukiendelea kuulizana baadhi ya mambo kwa maana ya kujuana vyema.
Siku moja nilimuomba Nancy anipe namba zake za simu ili tuweze kuwasiliana hata kwa meseji za kawaida na simu za kawaida kwani namba aliyokuwa anaitumia WhatsApp siyo namba ya Tanzania. Hapa pia nilizonga utata mkubwa sana kwani Nancy hakutaka kunipa namba.
"Namba nitakupa tu Samir wala usijali kwani tatizo nini Darling? Kama kuwasiliana mbona tunawasiliana kama hivi".
Nilimjibu Hapana Nancy kwanini hutaki kunipa namba zako au bado huniamini?
Baada ya Nancy kuninyima namba zake za simu, nilijiuliza maswali mengi sana kwamba kwanini Nancy hataki kunipa namba zake? Au hajanikubalia.?, atakuwa amenirizisha tu? Au bado haamini kama nampenda? Au hanipendi? Nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, hali hiyo ilinifanya nipunguze mapenzi sana. Nancy baada ya kugundua kuwa nimepunguza mapenzi kwasababu hiyo ilibidi anieleze ukweli ulivyo.
"Sikia Samir mpenzi wangu,ngoja nikwambie ukweli ulivyo.Yaani Mimi sipo Tanzania".

Dah! Baada ya kuambiwa hivyo nilipata mshangao kidogo moyoni kisha nikamuuliza upo nchi gani? Akanijibu "nipo Dubai"
"Upo Dubai?" "Ndiyo Samir"
Binafsi nilifikiri kuwa atakuwa amepata bwana mwarabu hivyo ameolewa. Niliumia sana bila kupata uhakika wa ninachokifikiri kisha nikamuomba anieleze kwa kina kwamba Dubai ameenda kufanya nini? yaani nilimtaka anihadithie kirefu.Nancy alinieleza kwa kina.
"Samir Mimi nilisomea hotel management. Kwahiyo Dada yake na Mubaraka (Wifi yangu) alinifanyia mpango wa kunitafutia kazi kwenye hotel fulani hivi Dubai, kwahiyo nipo huku sasa nina mwaka na zaidi najaribu kutafuta maisha".
Baada ya kunieleza habari hiyo. Nilizidi kuhisi kuwa bado kuna mahusiano mazuri yanaendelea baina ya Nancy na Mubaraka. Lakini sikutaka niruhusu mawazo hayo yaniumize sana moyoni mwangu, nilipuuzia tu na kukubaliana naye bila kuonesha tofauti ila nilijipanga kumuonesha mapenzi ya dhati Nancy ili aweze kumsahau mpenzi wake aliyezaa naye.
Basi mapenzi mubashara tulifanyiana, asikwambie mtu hakuna kitu kinaleta raha kama mapenzi yanapokuwa yanachipua kwa mbwembwe zote, ama kwa hakika nilifurahia sana kuingia katika mahusiano hayo bila shaka hata yeye alifurahia pia.
Nakumbuka tu tulivyokuwa tunakaribishana chakula kwa kurushiana picha. Mapenzi yalinoga! sijawai kuwa katika mahusiano niliyoyafurahia kwa kiasi kile.
Sijui nieleze vipi lakini niseme tu nilifurahia Sana.
Baada ya miezi mitatu hivi Nancy alifiwa na mtoto wa binamu yake, hivyo alitamani sana kuhudhuria mazishi ya msiba huo lakini kabla ya msiba huo kutokea marehemu alikuwa anasumbuliwa hivyo alilazwa kwa kuwa hali yake haikuwa nzuri. Nancy baada ya kupata taarifa hiyo ilibidi aniambie kwamba nimwambie boss wake kuwa nyumbani kuna mgonjwa amezidiwa sana.
Nilijifanya kama kaka yake na Nancy hivyo Nancy alinipa namba za boss wake ambaye niliwasiliana naye kwa kutumia lugha ya kiingereza kwasababu anafahamu kuzungumza lugha ya kiarabu na kiingereza tu.
Basi nilimueleza boss akanielewa, lakini baada ya siku mbili tu yule mgonjwa alifariki ilibidi nimuelekeze Boss kuhusu huo msiba na kwamba kulingana na mila na desturi zetu inabidi Nancy arudi mara moja ili aweze kuhudhulia mazishi hayo.
Bahati nzuri boss alikuwa muelewa sana, akanielewa nilichomueleza na akaniuliza kwamba atatumia muda gani? nilimjibu wiki mbili, basi akafanya mpango wa kupata tiketi ya ndege ambapo kesho yake saa tano asubuhi Nancy alisafiri kuja Tanzania.
Mara baada ya Nancy kupanda ndege sikuwa na mawasiliano naye tena kwani alizima simu na hata baada ya kuwasili Tanzania katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius  Nyerere jijini  Dar es salaam bado pia sikuwa na mawasiliano naye kwani ilibidi asajili line ya Tanzania ili tuweze kupata mawasiliano.
Alisajili line zake kisha akafanya utaratibu wa kupata usafiri haraka wa kutoka Dar kuja Ifakara alianza safari majira ya kama saa tano hivi asubuhi, baada ya kuwa ametulia vyema akiwa safarini alinipigia simu na kunitambulisha kuwa ameanza safari.
Alifika Ifakara muda wa saa tano usiku.Ambapo alichukua boda boda na kuelekea Mtaa wa Uhuru kwa mama yake. Alinitumia meseji kunijulisha kuwa amefika salama Ifakara na kwamba anaenda kwa mama. Asubuhi na mapema aliamka na kuelekea Msibani, nakumbuka siku hiyo hatukuweza kuwasiliana kutwa nzima mpaka giza lilipoingia, alidai kwamba simu yake iliisha chaji. Basi siku ya pili yake asubuhi muda kama wa saa nne hivi nilimtaka tuonane kwani tangu afike hatukuwai kuonana alikuwa yupo bize sana.
"Kwanini tusionane jioni Samir?"
Alisema Nancy nami nilimjibu kuwa nataka tuonane asubuhi hii ili twende hospitali tukapime afya zetu. Kwa maana ya kwamba tukapime AIDS virusi vya ukimwi ili tuwe katika mahusiano tukijiamini.
Nancy alikubali tukutane kisha tukaenda hospitali ya St Francis, nakumbuka tulipiga picha za selfie tukiwa kwenye benchi la wanaokaa watu wanaosubiri kuingia kwenye chumba cha daktari yaani kwenye foleni. Ilikuwa ni Picha ya kwanza kupiga na mrembo huyo Nancy.
Nilitamani tupige Picha nyingi zaidi lakini mazingira hayakuruhusu. Baada ya kutoka hapo Nancy alielekea nyumbani na Mimi pia nilielekea nyumbani. Unajua jioni yake nini kiliendelea?

Jioni ya siku hiyo, tulikutana sehemu fulani kisha tulitoka pale na kuelekea lodge. Huko tulipiga stori kwa kina kisha do me I do you yaani ule mchezo wa kikubwa, tuliufanya siku hiyo kwa uhuru mkubwa sana kwasababu vipimo vilionesha kuwa wote tupo salama.
Mambo yote hayo yaliyokuwa yakifanyika kwangu nilihisi kama nipo ndotoni. Nilikuwa siamini kama kweli nipo na Nancy kwa wakati ule maana ilikuwa ni kwa mara ya kwanza kufanya mapenzi na mrembo Nancy nimpendae kwa dhati. Asikwambie mtu, kufanya mapenzi na mtu unayempenda inaleta raha sana. Baada ya kumaliza kufanya mambo yetu tulivaa nguo kisha tulipiga Picha moja kali sana ambayo naikumbuka mara kwa mara kuitazama.
Hatukulala lodge siku hiyo bali tulitoka muda wa saa sita hivi kasoro dakika kadhaa. Nilimtafutia usafiri wa uhakika wa kumpeleka nyumbani, nami nilichukua boda na kurudi nyumbani.
Kila mmoja alioneshwa kufuruhishwa sana na mchezo ule tulioucheza last night. Hakika tulifurahia mno mchezo, asubuhi tulitumiana meseji.
Baada kama ya siku nne hivi Nancy alitakiwa kuondoka kuelekea Dar es salaam ili ajiandae na safari ya kwenda Dubai basi tuliwasiliana kuwa nimsindikize stand asubuhi. Tulikutana asubuhi hiyo na kumsindikiza stand, nakumbuka tulipofika stand tulipiga picha (selfie) huku tukitabasamu na kufurahi pamoja.

Hakika naikumbuka sana siku hiyo. Mara muda wa kuondoka ulifika tuliingia ndani ya gari na kumsindikiza mpenzi wangu huku tukipiga stori mpaka kibaoni kiasi kama cha kilometa tano hivi kutoka pale stand kisha nikashuka na kuchukua boda kuelekea nyumbani, ila nilitamani sana tuwe wote katika safari hiyo mpaka jijini Dar es salaam lakini kwa sababu za msingi ilishindikana. Nilidondosha chozi kisha na yeye baada ya kuniangalia pia akadondosha chozi, nikawa nashuka kwenye gari nilipofika mlangoni kabla ya kushuka ngazi nikampungia mkono kuashilia nilikuwa namuaga.
Baada ya hapo tulikuwa tunachati huku akiwa safarini. Alipofika Dar es salaam alinijulisha kuwa amefika salama. Kabla ya kupanda ndege kuelekea Dubai alikaa hapo Dar es salaam siku kama tatu hivi. Wakati yupo Dar Nancy alikuwa bize sana kiasi kwamba hata kuwasiliana na mimi ilikuwa inashindikana. Ubize huo uliniumiza kichwa sana kwasababu huko ndiko aliko mzazi mwenzake, sasa nilihisi kabisa kuwa muda huo wote asionitafuta mimi huwa anakuwa  na mzazi mwezake. Muda mwingine nilikuwa nampigia simu lakini alikuwa hapatikani na hata akipatikana basi alikuwa hapokei simu yangu. Mara chache sana alikuwa anapokea simu yangu nilipomuuliza kwanini anakuwa bize namna hiyo alinijibu tu kwamba anatembelea ndugu jamaa na marafiki, nilishtushwa sana na hali hiyo. Lakini  sikutaka kuibua migogoro ndani ya penzi letu kwani sikupenda na wala sikutamani kuona penzi letu linateteleka.
Basi ilifika siku ya kuondoka lakini kabla ya kuondoka usiku wa siku ambayo kesho yake alitakiwa kuondoka, aliniomba aende kulala kwa baba mkwe wake ambako huko ndipo anapokaa mtoto wake, mzazi mwezake pamoja na baba mkwe wake. Ukweli ni kwamba sikutamani kumruhusu lakini ilinibidi nifanye hivyo kwasababu najua hata nisipomruhusu haisadii kitu kwani anaweza kwenda kwa kunificha. Nilikuwa na hofu kubwa lakini yeye mwenyewe alijitahidi kunipa moyo kwa kunihakikishia kuwa atalala chumba tofauti na mzazi mwenzake.
Angalia jinsi kupenda kulivyokuwa na upofu mkubwa.Jambo kama hilo hata kwa kutumia akili ya kawaida tu haliwezekani kabisa lakini mimi kwasababu nilimpenda Nancy basi nilijitahidi kuvumilia hali hiyo kwa kuhisi labda kweli watalala vyumba tofauti.
Nakumbuka siku hiyo hatukuweza kuwasiliana vizuri na ilifika muda akawa hajibu meseji wala hapokei simu yangu. Hofu ilizidi kutanda pale alipoamua kuzima kabisa simu akawa hapatikani, kila nilipopiga simu nilijibiwa "namba unayoipigia haipatikani kwa sasa tafadhari jaribu tena badae".
Basi nilijiuguza maumivu yangu kimya kimya sikutaka kumuonesha Nancy tofauti yoyote ile na hata ikapelekea kuharibu penzi letu. Nilijitahidi kutunza na kulinda penzi letu lisiharibike.
Mara kukapambazuka akaanza safari ya kuelekea uwanja wa ndege kwaajili ya kuanza safari ya kwenda Dubai wakati huo wote anafanya michakato ya safari mimi hakunipa taarifa yoyote mbaya zaidi mpaka ameanza safari yake kuelekea Dubai mimi sikuwa na taarifa.
Dah! Niliwaza sana kwanini hali hii? Au kuna kitu kimemsibu na hata akawa hivyo. Lakini niliendelea kuwa mvumilivu na mwenye subira kwakuwa sikutaka kupaniki kwani ningeweza kumpoteza Nancy.
Basi baada ya kufika Dubai Nancy alinitafuta. Nilipomuuliza kuwa kwanini ameondoka bila kunipa taarifa yoyote akanijibu kwamba alikuwa ana haraka kwahiyo ile haraka haraka ndiyo iliyomfanya asiniage. Basi sikutaka tuibue mjadala zaidi nikaachana na swala hilo. Mapenzi yetu yaliendelea tena kung'aa vizuri yaani ilifika pahala nikaona kwamba ananifaa, hata yeye pia alinionesha mapenzi na kunifanya niwe karibu naye sana. Mapenzi mubashara yalinifanya nimkabidhi moyo wangu Nancy, sikusita kumuonesha mapenzi yangu ya dhati hata yeye pia alinionesha mapenzi ya dhati.
Basi raha na furaha hiyo ya mapenzi iliishi kwa muda wa miezi kadhaa. Baada ya kama miezi mitatu hivi mambo yalianza kubadilika. Hapa naomba niseme kitu kuwa Nancy alikuwa na simu mbili zote smartphone aina ya Samsung simu hizo zote zilikuwa zipo hewani kwa kutumia line tofauti lakini tulikuwa tunawasiliana sana kupitia line moja ambayo yeye mwenyewe aliiteua iwe kama ndiyo simu yetu ya mawasiliano. Hivyo alivyokuja Tanzania simu moja ile ambayo iliyokuwa haitumiki mara kwa mara alimpa bwana yake aliyezaa naye kama zawadi bila mimi kujua na wala hakuniambia kitu kama hicho.
Siku moja Mimi nilijisahau na kujikuta napiga namba ile kupitia IMO video call, nilistaajabu kusikia na kuona mwanaume ndiye aliyepokea simu kwani baada ya kupewa simu hiyo yeye hakubadilisha namba za WhatsApp na IMO aliendelea kutumia account ya Nancy. Hapa niseme tu niliumia sana tena sana.
Lakini bado sikutaka kumwambia Nancy na wala sikutaka hiyo iwe sababu ya mimi kugombana na Nancy.
Basi tukaendelea na mapenzi yetu kama kawaida lakini ikatokea siku nyingine tena nikajisahau nikapiga namba ile akapokea tena mwanaume hapo nilihisi maumivu yamenizidia na hata kumuuliza Nancy, lakini bado sikumuuliza kwa hasira ama kuonesha dalili ya kuchukizwa sana bali nilimuuliza kwa utaratibu tu. Nilimuuliza Nancy kuwa vipi mbona nimepiga namba yako ile nyingine amepokea mwanaume? Akanijibu kwa kutaka kuniongopea
"Hapana Samir labda umekosea tu mbona hii simu ninayo huku"
Nikamuuliza kwamba "una uhakika na jibu lako"
"Samir jamani tuachane na hiyo mada basi"
"Sipo tayari kuachana na hiyo mada mpaka nipate majibu yakinifu"
Basi alirukaruka sana kisha akaniomba msamaha na kuniambia kwamba ile simu yeye alimwachia mtoto wake(Athman) ambaye ana umri wa miaka mitatu kwamba alikuwa anamlilia sana hivyo alimwachia ili amtoroke kwa wepesi. Kwahiyo yeye alivyoiona ndiyo ameichukua na kuitumia so please and please forgive me kwa hilo Darling "
Ukweli ni kwamba niliumia sana tena sana kiasi kwamba siwezi kuelezea lakini kwakuwa nilikuwa bado nampenda sana Nancy basi sikutaka kufanya debate juu ya suala hilo nikaachana nalo. Maisha yaliendelea kunoga kwa kipindi kama cha wiki mbili hivi kisha Nancy alianza kuonesha dalili za kuchoka mapenzi yetu hivyo alianza kufanya vitiba mbali mbali.

Siku moja aliniambia nimtumie picha ya mpenzi wangu. Kama ambavyo nilivyoeleza hapo awali kuwa sikumficha nilimueleza bayana kuwa nina mpenzi kama ambavyo yeye alivyonieleza juu maisha yake ya mahusiano. Alipotaka nimtumie picha ya mpenzi wangu nilimkatalia kwa hekima kumueleza kwamba sina picha yake lakini hata hivyo alitambua bayana kuwa nimemkatalia na kulazimisha nimtumie, Mimi pia sikutaka kumtumia basi alininunia na kukata mawasiliano na Mimi kwa muda wa siku kama mbili. Kisha akaanza kunitafuta na kuniambia kwamba.
"Naomba nisamehe Samir Mimi nilifanya vile ni wivu tu ulionisukuma, lakini nakiri kweli nimekukosea Samir please naomba nielewe mpenzi wangu".
Mimi sikuwa na tatizo naye aliponiomba msamaha basi tukaendelea na safari yetu ya mapenzi lakini hayakuwa na afya kama ambavyo ilivyokuwa hapo zamani. Hazikupita siku nyingi sana akazua tena suala jingine. Safari hii aliniuliza swali
"Hivi Samiri unampenda huyo mpenzi wako uliyenaye?"
"Nancy achana bana na hayo maswali"
"Hapana Mimi naomba unieleze Samir"
"Sawa ndiyo Nampenda".
" Aah! Sawa nashukuru kufahamu hilo".

Basi baada ya hapo vituko vilikuwa vingi sana mpaka akawa anaweka status na profile pictures za mafumbo kwenye account yake ya WhatsApp. Bado akaona haitoshi akawa ananitumia baadhi ya meseji za kuonesha mimi kama vile simpendi kwa dhati. Siku moja akatuma meseji ya wazi kabisa kunishutumu kuwa sina mapenzi ya dhati kwake, kwakweli niliumia sana nikawa sifahamu nifanye nini ili ajue kama kweli nampenda. Basi kila tunapochati ikawa haipiti siku bila kugombana ama kupishana kauli. Ilifika pahala tukachuniana kama siku tano hivi bila kuchati.
Mara yeye akaanza kunitumia meseji "Mambo baby!". Kabla ya mimi sijajibu akatuma tena meseji nyingine." Samahani Samir"
"Samahani ya nini Nancy?"
"Kwa kukuita baby"
"Kwahiyo Mimi siyo baby wako?"
"Tuachane na hiyo mada Samir"
"Hapana Nancy natamani nijue hilo"
"Sawa, kwa mfano swali hili ningekuuliza wewe ungenijibu vipi?"
"Nancy mbona unakwepa swali, okay wewe ni my baby. Haya niambie sasa kutoka kwako".
" Mimi Hapana"
"Hapana!!!"

Nilishangazwa sana na jibu la Nancy la kunijibu hapana mimi sio baby wako kisha akanitumia voice note iliyokuwa ikieleza kuwa
"Samiri tusifanye vitu kama watoto,unajua mtu anapokutaka hata kama hajakutongoza unaweza kuelewa tu kwamba anakupenda vivo hivyo hata kama mapenzi yamechujika utaelewa tu sio mpaka mtu akwambie. Mimi naona dhahili kuwa mapenzi yamechujika na kwamba sasa hivi kila mmoja awe huru kufanya mambo yake. Wewe kuwa huru kufanya mambo yako na mimi niwe huru kufanya mambo yangu, hivyo yaani".
Dah! Uamuzi wake huo nilishindwa kuelewa sababu hasa ni ipi na hata akafikia huko, maana huo ni uamuzi mgumu sana ila nilikubaliana na uamuzi huo japo uliniumiza sana, kimsingi nilikuwa nafikiria sana nitawaeleza nini baadhi ya marafiki zangu wa karibu niliowahakikishia kuwa huyu ndiye shemeji yenu, nitawaambia nini wazazi wangu hususani mama ambaye nilimueleza bayana kuwa yeye ndiye mke wangu mtarajiwa na hata alivyokuja kwenye msiba Ifakara alifika mpaka nyumbani na kusalimiana na mama yangu. Nitamueleza nini mama?. Lakini mbaya zaidi nitaueleza nini moyo wangu ambao pia uliamua kutulia kwake na kujihakikishia kupata kambi ya kudumu milele kutoka kwake. Nitayaeleza nini macho yangu yaliyorizika na kupedezwa kuona uso wake, kifua chake, matiti yake na hata mapaja yake.
Hapo ndipo nilipoanza kupata picha nzima sasa kwanini alinizuia nisimpost Facebook kumbe alikuwa hayupo tayari kuwa na Mimi!, hapo ndipo nilipogundua kuwa kwanini alikuwa hataki mahusiano yetu yawe wazi, hapo ndipo nilipogundua kuwa kwanini alikuwa hataki nimuweke hata dp WhatsApp. Kumbe alikuwa hayupo tayari kuishi na mimi, lakini nashukuru nimeujua ukweli kutoka kwako mapema kabla hatujafika hatua ya ndoa kama ambavyo tulivyopanga, tunapanga kufunga ndoa kumbe mwenzangu alikuwa na mpango wake. Bora ungeniambia mapema Nancy ningejua nisingezama katika kina kirefu namna hii na hata nashindwa kutoka sasa. Tazama thamani ya machozi yangu yanayotoka kwaajili ya maumivu ya penzi lako.
Leo nimeandika stori hii kwaajili yako Nancy najua utaipata na kuisoma hata kama utachelewa kuipata lakini ni matumaini yangu kuwa utaisoma Simulizi hii kwaajili yako Nancy.
Nancy hivi unakumbuka mambo mangapi mabaya ya kukithiri niliyowai kukufanyia na hata ukaamua uamuzi huu. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Najua mimi ni mnyonge sana kiuchumi  kushinda hata jamaa uliyezaa naye huenda hiyo ikawa sababu lakini hukumbuki hata mazuri yangu machache niliyowahi kukufanyia kabla hujafanya uamuzi huu. Nancy sikulaumu kwa uamuzi wako najua huo ni uamuzi wako na siwezi kukulazimisha ubaki na mimi kwani mapenzi hayalazimishwi. Sawa nenda Nancy.
Nancy nenda ingawa kishingo upande lakini najua kisichoridhiki hakiliki, nilijitahidi sana kukufanya uwe wangu lakini imeshindikana umeamua kwenda Nancy, naumia sana kwani yapo mambo pia uliwahi kunifanyia ambayo yatanifanya nizidi kukumbuka na kuhitaji uwepo wako ninaumia sana na nitaumia sana lakini kwa hatua hii uliyofikia ni bora uende Nancy, nitajitahidi kusahau, sawa nimeumia ila nitazoea but tambua Nancy maisha duara ipo siku nawe yatakutokea.
Lakini Nancy Mimi nakumbuka tu nilivyokuwa najaribu kukuimbia japo sio msanii lakini nilifanya hivyo kwaajili yako nilikubembeleza kwa kukuimbia nyimbo za mahaba ili niweze kukufurahisha na kukufanya ufurahie mahusiano yetu "wow! Jamani baby una sauti nzuri! Nina enjoy sana kuwa na wewe habibi wangu" hivi ndivyo ulivyokuwa unanieleza baada ya kukuimbia. Je na wewe unakumbuka?
Nancy nakumbuka pia jinsi tulivyokuwa tunazungumza kupitia mtandao wa IMO huku tukionana nyuso zetu na kuoneshana tabasamu bashasha. Je na wewe unakumbuka?
Nakumbuka jinsi tulivyokuwa tunatumiana picha. Nazikumbuka sana zile picha tulizopiga stand siku niliyokuwa nakusindikiza ulipokuwa unatoka Ifakara kuelekea Dar es salaam, nakumbuka sana pia zile picha tulizopiga St Francis siku ile tuliyoenda kupima afya (VVU). Nakumbuka tulivyokuwa tunakaribishana chakula je na wewe unakumbuka Nancy?
Nilifurahi sana siku tuliyokwenda hospital kwaajili ya kupima virusi vya ukimwi (VVU) na wote tukabainika kuwa tupo safi Yaani hatujaathirika. Nilitamani nipate mbeleko nikubebe mgongoni kutwa nzima ili kuonesha furaha yangu lakini haikuwezekana kwasababu siku hiyo ulikuwa upo bize sana. Nilimaliza majina yote mazuri ya kuwaita wapenzi nilikuita lakini bado nikahisi haitoshi nikawa nazidi kutafuta vitu vya kukufanyia ili kuonesha upendo wangu kwako.
Je vipi kuhusu zile nyimbo za mapenzi tulizokuwa tukitumiana zenye ujumbe adhimu kabisa kwaajili ya kusifiana na kupambana. Nancy, do you remember?
Lau kama ungejua ni kwa jinsi gani umeumiza moyo wangu hakika ungenionea huruma, nilikukabidhi moyo wangu wote, umeshindwa kuutunza, umeshindwa kuuhifadhi moyo wangu. Matokeo yake umeutia majeraha, umeupa vidonda, nimepata ajari ya kupenda lakini nitajitahidi kuuguza kidonda changu.
Nakumbuka vitu vingi sana Nancy kutoka kwako. Lakini pamoja na kuwa sasa hivi tumeachana ila mimi siwezi kukusema vibaya hata kwa yale mazuri uliyonifanyia. Sijutii kukufahamu maana nimejifunza mengi na nimefurahia vingi kutoka kwako.
Nimeandika walaka huu nikiwa na simanzi kubwa la kuvunjika kwa mahusiano yetu lakini najua ni makusudi ya Mungu ni bora nimekugundua mapema kabla sijafunga nawe pingu ya maisha. Ni vyema umenionesha wewe ni nani, sasa nimekutambua Nancy. Nitamtafuta anipendaye kwa dhati niishi naye kwa amani. Kama walaka huu utakuwa umekukera Nancy basi natanguliza I'm sorry yangu kwako na kama utakuwa umenielewa nilichomaanisha na ukatambua makosa uliyonifanyia basi chukua somo ujifunze ili utulie na uishi kwa amani na huyo umpendaye. Nakutakia maisha mema Nancy.








Usikose kufuatilia Msimu wa pili wa NAKUMBUKA TU

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MAPENZI NI MAWASILIANO

SIMULIZI YA NAKUMBUKA TU NA AWADH PALANGU